ZIARANI SUMBAWANGA

dismas ten

JUMLA ya nyota 25 wa kikosi cha Mbeya City Fc asubuhi hii wanaanza safari kuelekea wilayani Sumbawanga tayari kwa ziara ya michezo minne  ya kirafiki ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya  mchezo wa ligi kuu ya soka Tanzania bara dhidi ya Young Africans uliopangwa kuchezwa Mei 14, kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Muda mfupi uliopita  Afisa habari wa kikosi hiki, Dismas Ten ameidokeza mbeyacityfc.com kuwa kutokana na umuhimu wa mchezo wa Dar es Salaam,benchi la ufundi chini ya kocha mkuu Kinnah Phiri liliona kuna haja ya kutafuta michezo ya kirafiki kwenye eneo ambalo hali ya hewa  inafanana na iliyopo uwanja wa Taifa ili kutengeneza  mazingira mazuri kwa wachezaji ambao muda mwingi wamekuwa wakifanya mazoezi kwenye baridi.

Tumekuwa tukifanya mazoezi kwenye maeneo yenye baridi, mchezo ujao tunacheza uwanja wa taifa eneo ambalo hali ya hewa iko tofauti na tuliyoizoea, hivyo basi benchi la ufundi likaona kuna haja ya kwenda Sumbawanga kufanya maandalizi zaidi kwa sababu eneo hilo hali yake ya hewa inafanana na iliyopo jijini Dar.

 

Hivyo basi jumla wachezaji 25 watasafiri wilayani humo tayari kwa michezo hiyo ya kirafiki  na baada  ya hapo kikosi kitarejea Mbeya kwa matayarisho ya mwisho kabla ya kusafiri Dar kwenda kuikabili Young Africans.

Katika hatua nyingine Ten amedokeza kuwa City haihusiki na taarifa zinzosambaa hivi sasa kwenye mitandano ya kijamii ikihusisha kikosi chake na kutaka kumchukua kocha wa Mbao Fc ya Mwanza Etiene Ndayilagije.

Kama klabu hatujatamka popote juu ya kuwepo suala hilo, sisi bado tuna kocha wetu ambaye tulisaini naye kandarasi ya miaka mitatu hivyo basi hakuna taarifa yoyote kwa sasa kuhusu kocha Etiene, ni ngumu kuzuia watu kuzungumza kwenye mitandao ya kijamii kwa sababu ni sehemu yao lakini ukweli kutoka kwetu ni kuwa kocha Kinnah Phiri bado ataendelea kuwa kwenye benchi la ufundi la timu yetu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *