Mohamed Mkopi dakika 365…

1200X600

Mshambuliaji wetu Mohamed Mkopi aliye hapa shinyanga na kikosi cha Mbeya City FC kinachojiandaa na mchezo nambari 41 dhidi ya Mbao FC katika uwanja wa CCM Kirumba, amezungumza na www.mbeyacityfc.com mapema leo hii baada ya mazoezi ya asubuhi yaliyosimamiwa na Kocha Ramadhani.

Mkopi aliyecheza kwa jumla ya dakika 365 mpaka sasa, na ambaye katika mchezo uliopita aliweka wavuni goli lake la kwanza akiwa na jezi ya dhambarau panapo dakika ya 78 ya mchezo, ni sehemu ya nyota wengine 23 waliosafiri kuja hapa kanda ya ziwa kupambana katika michezo mitatu ya ugenini dhidi ya Stand United, Mwadui na kisha 13.10.17 dhidi ya Mbao.

Kuhusu kocha mpya

‘Mwalimu Ramadhani tumeanza naye leo katika mazoezi ya asubuhi hapa Shinyanga, na tumeona makali yake kwa macho yetu. Mtindo anaotumia kufundishia, namna na jinsi anavyotuonesha kwa mifano ni ishara tosha kuwa msimu huu utakuwa moto sana kwa City’. Alisema Mkopi juu ya mwalimu mpya wa klabu yetu Kocha Nsanzurimo Ramadhani. Mwalimu Ramadhani baada ya kuwasili wiki iliyopita, leo hii ameanza rasmi kukinoa kikosi chetu kilichokua chini ya Mwalimu Kijuso toka kuanza kwa ligi kuu msimu huu.

Matarajio yake

Akiwa miongoni mwa wachezaji wenye mafanikio uwanjani kwa kupachika magoli mengi katika ligi kuu Tanzania bara, Mkopi anafurahi kuwa sehemu ya kikosi hiki baada ya kukosa kuitumikia klabu msimu wa 2016/17. ‘Nilivumilia msimu mzima baada ya bodi ya ligi kunipatia hukumu ya kutojihusisha na soka kwa msimu mzima, wakati wote wa adhabu yangu nilikua na maumivu lakini sikuwa na namna zaidi ya kuwa mvumilivu na kusubiri wakati ufike. Na nina imani huu ni wakati bora zaidi kwangu na nina matumaini baada ya kupachika wavuni goli langu la kwanza katika mchezo uliopita dhidi ya Mwadui, neema ya magoli itaanza kumiminika kwangu binafsi na kwa wachezaji wenzangu wote. Ninataraji kuwa msimu huu tutafunga magoli mengi na kuipatia pointi nyingi timu yetu.’

Shirikisho , usimamizi wa ligi na mpira kwa ujumla

Mohamed Mkopi pia alitoa maoni yake na ushauri kuhusu usimamizi na uendeshaji wa ligi hapa nchini ‘Ninaomba sana msimu huu bodi ya ligi iwe makini zaidi, kwa kusimamia vema ligi yetu kwa maendeleo ya vilabu na Taifa kwa ujumla. Usimamizi wa ligi ukiwa bora, tutaweza toa wachezaji wengi wenye vipaji na hatimaye kukuza timu yetu ya Taifa. Mimi nilifungiwa msimu mzima kwa tuhuma za kusajili timu mbili kwa wakati mmoja, adhabu ambayo haikua sahihi kwa sababu shauri langu halikupata muda kusikilizwa. Mapema msimu huu tumeona kabisa mchezaji wa timu kongwe akikiri kusaini timu mbili kwa wakati moja lakini kazi na taaluma yake ya mpira ikalindwa. Lakini hili ni kosa ambalo mimi binafsi nilituhumiwa na sikusikilizwa vema kwa kuwa haikua sahihi kabisa. Busara hii ingetumika kwangu, ingekua ni nafasi nzuri kwangu na nina imani msimu ulioisha ningekua nimeitumikia timu yangu kwa ufanisi mkubwa na kuipatia matokeo. Kusimama kwangu kwa msimu mzima kumepungua ufanisi wangu na inanigharimu sana kurudi katika hali yangu ya kawaida.’ alimalizia Mohamed Mkopi

Ligi kuu imesimama mpaka hapo tarehe 13.10.17 ambapo City itashuka dimbani kupambana na Mbao FC ya Mwanza. Wakati wote huu kikosi kinabaki hapa Shinyanga kujiandaa na mchezo huo.

Shah Mjanja
MCCFC

Ulipitwa na mahojiano aliyofanya Fikirini Bakari? Tazama hapa chini golikipa huyu nambari mbili akiwahoji wachezaji wenzake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *